MAPEMA TU KAZI ISHAISHA TAIFA, MIFUMO NA MBINU ZA MAKOCHA WOTE WA YANGA NA AZAM FC NI PACHA

MAPEMA TU KAZI ISHAISHA TAIFA, MIFUMO NA MBINU ZA MAKOCHA WOTE WA YANGA NA AZAM FC NI PACHA. 
ITAFAHAMIKA leo baada ya dakika 90 zile tambo za Yanga na Azam FC ambazo zilikuwa zinatawala kwa kila mmoja kuvuta kwake Uwanja wa Taifa.
Mashabiki watakuwa wameshatambua nani atakuwa mbabe leo ataongeza hatua mbele hasa ukizingatia kwamba vita ya nafasi kwa sasa ni kubwa.
Yanga iliyo chini ya Kocha Mkuu, Luc Eymael raia wa Ubelgiji ikiwa nafasi ya tatu na pointi 55 itamenyana na Azam FC iliyo chini ya Mromania, Aristica Cioaba iliyo nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 zote zimecheza mechi 29.
Mbinu za Mbelgiji wa Yanga
Kocha Eymael kwenye mazoezi yake ya hivi karibuni amekuwa akiwanoa wachezaji wake kufunga mabao ya ndani ya 18 ili kupata ushindi.
 Eymael ameliambia Spoti Xtra kuwa ana matumaini wachezaji wake wataingia uwanjani wakiwa na hesabu za kulipa kisasi.
“Nina amini utakuwa ni mchezo mzuri na wachezaji wangu wataingia uwanjani wakiwa na hesabu za kulipa kisasi ukizingatia kwamba kwenye mchezo wetu uliopita tulipoteza kwa kufungwa.
“Halafu ajabu ni kwamba goli lenyewe ni la kwetu wenyewe, kiuhalisia hawajatufunga, tulijifunga wenyewe,sasa hapo nadhani unaona namna jinsi mchezo utakavyokuwa mzuri, tunahitaji ushindi hakuna jambo jingine.
 Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ameliambia Spoti Xtra kuwa Kocha Mkuu, Cioaba amegawa majukumu kwa wachezaji wake wote ili kuona wanapata matokeo chanya.
“Tupo tayari na maandalizi yetu yalianza tangu Mei 27. Tulipocheza na Mbao FC na kushinda mabao 2-0 ulikuwa ni mwanzo wetu wa kuendelea kujiandaa kwa ajili ya Yanga.
“Wachezaji wanajua kwamba tukishinda mechi yetu tunajihakikishia kukaa nafasi ya pili,tutafanya kitu cha kipekee na wengi hawataamini.”
Mifumo yao pacha
Eymael wa Yanga na Cioaba wa Azam FC wote wanaonekana kupenda kutumia mfumo wa 4-4-2 kusaka ushindi.
Eymael mechi zake mbili za Ligi Kuu Bara mbele ya Mwadui FC Uwanja wa Kambarage na ule dhidi ya JKT Tanzania Uwanja wa Jamhuri alitumia mfumo huo.Cioaba kwenye ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Mbao FC alitumia mfumo wa 4-4-2.
Pia wakiamua wanatumia mfumo wa 4-3-3 kwenye mechi yao iliyochezwa Januari 18 wote walitumia mfumo mmoja.
Heshima ya rekodi
Mshindi wa leo anajiongezea heshima na kuweka rekodi mpya ya kushinda mechi nyingi zaidi ya mwenzake. Kwa sasa timu zote zimeshinda mechi nane nane hivyo mshindi atajiwekea heshima ya kuwa kinara kwa kushinda mechi nyingi.
Mechi ya kisasi
Mchezo wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Taifa, Yanga ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na beki wa Yanga, Ally Mtoni hivyo leo Yanga wataingia kwa lengo moja la kulipa kisasi.
Rekodi zinaonyesha kuwa tangu Azam FC ipande daraja msimu wa 2008/09 zimekutana kwenye mechi za Ligi Kuu Bara mara 23.
Azam FC imeshinda mara nane sawa na Yanga na zimetoka sare mechi saba.
Mechi zao za misimu minne ya hivi karibuni yalipatikana jumla ya mabao 17 ambapo Yanga ilifunga nane huku Azam FC ikifunga mabao tisa. Na timu iliyoshinda mabao mengi ilikuwa ni Azam FC ambapo ilifunga jumla ya mabao 3 kwenye mchez mmoja.
matokeo yao yapo hivi
2015/16
Azam FC 2-2 Yanga
Yanga 1-1 Azam FC
2016/17
Yanga 1-0 Azam FC
Azam FC 0-0 Yanga
2017/18
Yanga 1-3 Azam FC
Azam FC 1-2 Yanga
2018/19
Yanga 0-2 Azam FC
Azam FC 0-1 Yanga

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MATOKEO YA MECHI ZOTE NDANI YA LIGI KUU BARA

SIMBA SC KUMPA KICHAPO MWADUI FC